Khutba ya Ijumaa Masjid Al-Ghadir: Sheikh Hemed Jalala Aeleza Misingi ya Kuimarisha Imani na Mapenzi kwa Imam Hussein (AS)
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Swala ya Ijumaa ya tarehe 15 Agosti 2025 imeswaliwa katika Masjid Al-Ghadir, Kigogo Post, Jijini Dar es Salaam, ikiongozwa na Khatibu Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge.
Katika khutba yake, Sheikh Hemed Jalala amesisitiza umuhimu wa kuimarisha misingi ya imani na kuongeza kiwango cha imani kupitia matendo mema na ibada mbalimbali. Ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yanayoongeza imani ni:
1. Kuswali rakaa 51 kwa siku.
2. Kuswali Swala za Usiku.
3. Upendo na kumuenzi Maulana Sayyid Al-Shuhadaa, Imam Hussein (AS).
Akifafanua zaidi kuhusu mapenzi kwa Imam Hussein (AS), Mjukuu wa Mtume Muhammad (SAWW), Sheikh Hemed amesema:
“Ukilisoma tukio la mapinduzi ya Imam Hussein (AS) kama tukio la vita kati yake na Yazid bin Muawiya na ukaishia hapo, basi bado hujamjua Hussein (AS). Tukio la Karbala ni mapambano makubwa baina ya Haki na Batili. Siku ya A’shura, Mwenyezi Mungu aliinusuru Haki kupitia Imam Hussein (AS) na masahaba wake waliotoa maisha yao wakitetea Haki na kupinga Batili. Mapambano hayo yanaendelea kila kona ya dunia, na kila siku ni Siku ya A’shura.”
Maulana Sheikh Hemed Jalala pia ameeleza kuwa kila mwaka, wapenda Haki na wapinga Batili humtembelea Imam Hussein (AS) katika Ardhi ya Karbala, Iraq. Mwaka huu 2025, vyombo vya habari vya Iraq vimeripoti kuwa zaidi ya watu milioni 25 wameshiriki katika Ziara ya Arubaini.
“Mamilioni hawa kutoka pembe zote za dunia hupata huduma bure ikiwemo chakula, malazi, maji, tiba na mahitaji mengine ya msingi. Ziara ya Arubaini ni muujiza mkubwa wa Mwenyezi Mungu na ishara ya nguvu na ushindi.”
Aidha, Sheikh Hemed Jalala amesema katika ziara ya mwaka huu, Mazuwwari wa Imam Hussein (AS) wamewaombea watu wa Ghaza na Palestina kwa amani, utulivu na ushindi dhidi ya maadui wao.
“Insha Allah Mwenyezi Mungu atainusuru Ghaza na watu wake,” amehitimisha Sheikh Hemed.
Your Comment